Pia serikali imetangaza kufanyika kwa udahili upya Vyuo Vikuu vyote nchi nzima ili kuwaondoa vyuoni wanafunzi wote wasio na sifa sambamba na kutangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo ya elimu ya juu.
Hayo yamebainishwa leo na Prof. Joyce Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipozungumza na waandishi wa habali juu ya kuvunjwa kwa Kamishina ya TCU.
Amesema, kwa idhini aliyopewa na rais anawasimamisha kazi mara moja watendaji hao wa Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu.
Prof. Ndalichako amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Prof. Yunus Mgaya, Katibu Mtendaji wa TCU kwa kushindwa kusimamia kazi za TCU akiwa kama mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.
Pia, Dk. Savius Maronga, Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya Vyuo Vikuu.
Amesema Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Udahili amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kupelekea kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa, na mwingine aliyesimamishwa ni Kimboka Istambuli ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka.
Mbali na hilo Prof. Ndalichako amesema, ili shughuli za TCU ziendelee, Prof. Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mtendaji na kabla ya uteuzi wa kukaimu nahfasi hiyo Prof. Mwageni alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Aidha ameteuliwa Dk. Kokubelwa Mollel ambaye atakaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hiyo Dk. Kokubelwa alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa.
Waziri amesema, kutokana na hilo serikali imeamua kutoa tamko baada ya ukaguzi kufanyika katika chuo hicho katika kampasi za Arusha na Songea na kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa katika utoaji wa elimu isiyokuwa na kiwango.
Amesema, walibaini kuwepo kwa wanafunzi 489 ambao wapo katika vyuo hivyo ambao hawakidhi viwango na hawana sifa za kusoma Chuo Kikuu.
Amesema kibaya zaidi ni kuwepo kwa wanafunzi ambao ni wa kidato cha nne waliofaulu Daraja la Nne huku wengine wakiwa na pointi 32 lakini wakidahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
“Mwanafunzi wa Kidato cha Nne anasoma digrii ya Sayansi, huku mtu huyo akiwa sekondari kasoma mkondo wa biashara lakini kadahiliwa asomee Sayansi na analipiwa mkopo na TCU.
“Si tu hana sifa ya kusoma Chuo Kikuu, hana hata sifa ya kuwa na cheti cha ualimu kwa maana hiyo mtu wa aina hiyo hafai hata kuwa na cheti cha ualimu hatuwezi kukubali mtu wa jinsi hiyo akasomee digrii,” amesema.
Prof. Ndalichako amesema rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu lakini cha kusikitisha kuna wanafunzi waliofaulu vizuri Kidato cha Sita wanakosa mikopo ila wale waliofeli wanapata mikopo hiyo.
“Divisheni four pointi 34 yuko Chuo Kikuu hata ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” amesema.
Amesema, baada ya serikali kufunga chuo hicho wanafunzi hao walihamishiwa vyuo vingine lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya nyuma.
‘Wanafunzi waliotoka St. Joseph na kupelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka wa pili na wa kwanza wamerudishwa nyuma muhula moja huku wale wa mwaka wa tatu wamerudishwa nyuma mwaka moja” amesema.
Amesema, wale wa St. Joseph Tawi la Songea waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA) waliokuwa wakisoma mwaka wa nne wamerudishwa mwaka wa tatu na wametengewa vipindi vya ziada ili kurekebisha upungufu huo, na hata wale waliopelekwa vyuo vingine vya Ruaha, Mkwawa wameonekana kuwa na upungufu pia.
“Kibaya zaidi hao wanafunzi walikuwa wanapata mikopo, Division four anapata mkopo haki iko wapi, tulipoona jambo hili si sawa, tulichukua hatua tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo halikufanyika,” amesema.
Kufuatia kuwepo kwa matatizo hayo Prof. Ndalichako ametangaza vita kwa vyuo mbalimbali ambavyo vina watu ambao wanadahili wanafunzi wasio na sifa.
Kuhusu wanafunzi ambao hawakuwa na sifa lakini walikuwa wakisoma chuo kikuu hicho amesema licha ya kuwa wamepoteza muda wao mwingi lakini watalazimika kurejesha mikopo hiyo.
“Wale wote ambao walipata mikopo bila kuwa na sifa watarejesha mikopo hiyo na hakuna njia yoyote ya kuwasaidia bali wanatakiwa kuendelea kuangalia ni jinsi gani ya kujiendeleza,” amesema.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment