Dar/Zanzibar. Wakati Profesa Ibrahim Lipumba akieleza hawezi kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad hayupo, katibu mkuu huyo amerejea nchini jana tayari kwa baraza hilo litakalofanyika leo.
Baraza hilo linakutana kwenye ofisi za CUF, Vuga mjini Unguja likitarajiwa kutoa uamuzi ambao kwa vyovyote, utatoa taswira mpya kuhusu mgogoro uliojitokeza hivi karibuni ndani ya chama hicho hasa baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutangaza kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho na kufuta uamuzi wa mkutano mkuu maalumu wa kuwasimamisha na kuwafukuza uanachama baadhi ya viongozi wake.
Kikao hicho pamoja na mambo mengine, kinatarajiwa kupokea na kujadili ajenda iliyowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya CUF ya kumfikisha mbele ya baraza hilo Profesa Lipumba ili kujieleza kwa vitendo anavyoendelea kuvifanya dhidi ya chama hicho.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Bimani iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari mjini Unguja imesema tuhuma dhidi ya Profesa Lipumba ni pamoja na kuongoza kundi aliloliita la wahuni kuvunja ofisi, kupiga na kujeruhi walinzi wa chama kwenye ofisi kuu Buguruni.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, kwa kuzingatia masharti na matakwa ya Ibara ya 12(6), (7), na (16) ya katiba ya CUF ya mwaka 1992, toleo la mwaka 2014, kamati ya utendaji imeitisha kikao hicho ili kumpa fursa ya kujieleza na kujitetea kabla ya kuchukua hatua dhidi yake kwa lengo la kulinda heshima ya chama na kutunza nidhamu ya wanachama wote.
Baada ya baraza hilo kuitishwa, Profesa Lipumba alisema hatahudhuria kwa kuwa mwenyekiti wake ni Maalim Seif akisema yuko nje ya nchi na kwamba aliyepaswa kukaimu nafasi hiyo ni naibu katibu mkuu (Bara), Magdalena Sakaya ambaye naye hakushirikishwa. Hata hivyo, Maalim Seif alirejea nchini jana kimyakimya na kupokewa na baadhi ya maofisa wa CUF mjini Unguja.
Msimamo wa Lipumba
Jana, Profesa Lipumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba anamsubiri Maalim Seif arejee ili wazungumze huku akiwataka wanachama kuungana kukijenga chama hicho.
“Kama ni mgawanyiko, kweli huo upo na ndiyo changamoto tuliyonayo ya kuwaleta pamoja viongozi wa chama chetu. Wanachama tusiwe na mgawanyiko wa Watanzania Bara na Wazanzibari, tuwe chama kimoja. Hili ni jambo la muhimu sana la kulifanya na ni matarajio yangu. Natarajia katibu mkuu akirejea tuweze kufanya kazi pamoja,” alisema Profesa Lipumba.
Huku akitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani wa mwaka 2008 ambao Rais Barrack Obama alichuana na Hillary Clinton na Joe Biden katika chama cha Democratic na aliposhinda, aliwateua wawili hao kumsaidia.
“Hiki ni chama cha kiliberali, linatokana na neno ‘liberty’ yaani uhuru, chama kinachosimamia haki. Katika mambo ya kisiasa, kuwa na migongano ni jambo la kawaida, sasa tusiitafsiri kuwa uadui,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Tunayo kazi kubwa ya kuwaleta wana CUF wote pamoja na ninaomba wana CUF wote wa Zanzibar na Bara tumetoka mbali... Maalim Seif mimi nimekutana naye mwaka 1973 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa hiyo tunafahamiana siku nyingi, namwomba Mwenyezi Mungu jambo hili tulitatue,” alisema.
Amng’ang’ania Lowassa
Akizungumzia kujiuzulu kwake, Profesa Lipumba alirejea maneno yake kuwa nafsi yake ilimsuta.
“Lakini nilisema... siwezi kuwa mpigadebe wa Edward Lowassa. Mimi ni Profesa, Lowassa alikuwa mwaka mmoja nyuma yangu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa anafanya shahada ya sanaa. Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Tanu Youth League (sasa Umoja wa Vijana wa CCM – UVCCM), Lowassa alikuwa mwanachama wangu, kwa hiyo namfahamu siku nyingi,” alisema na kuongeza:
“Sasa nikasema hapana, nafsi yangu inanisuta, Profesa Lipumba awe mpiga debe wa Lowassa! Nikasema suala hilo siliwezi, ndiyo nikawa nimeng’atuka.”
Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu Agosti 5, 2015 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na nafasi yake kushikiliwa kwa muda na Wakili Twaha Taslima kabla ya kutengua uamuzi huo Juni 8, alikanusha kukitelekeza chama hicho huku akisema alijua Maalim Seif alikuwa karibu na Chadema hivyo alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kulinda masilahi ya chama hicho hususan majimbo waliyoachiwa katika Ukawa.
“Suala la chama chetu kupata wabunge 10 ni matokeo ya kuwekeza kwa muda mrefu na wanachama wanajua. Ukienda Kanda ya Kusini, ukienda Mtwara, Tanga wanajua, tumefanya kazi hii kwa muda mrefu,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo ndugu zangu wa CUF nawaeleza, mimi sikuwaacha katika wakati mgumu kwa sababu ningefanya hivyo labda mngekuwa mmeniteua mimi kuwa mgombea urais halafu dakika ya mwisho nikasema siwezi kuwa mgombea, ningekuwa nimewaacha kwenye wakati mgumu.”
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment