Watafiti hao waliuawa juzi kwa kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa moto. Gari la Serikali aina ya Toyota Hillux, pia lilichomwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa kijiji.
Alisema mwenyekiti wa kitongoji alipigiwa simu na mmoja wa wanawake waliokuwa eneo la tukio kwamba kuna wanyonya damu wamevamia kijiji.
Mambosasa alisema kwa kuwa mwenyekiti huyo alikuwa mbali, alimpigia simu mwenyekiti wa kijiji aende eneo la tukio kujua kilichotokea. Alisema mwenyekiti wa kijiji alipofika hakuamini maelezo ya watafiti hao na kuanza kuwashambulia.
Mambosasa alisema mtu mwingine alikwenda kijijini na kumueleza mchungaji wa kanisa kuhusu kijiji kuvamiwa na nyonya damu, naye akatagaza kwenye kipaza sauti kwamba kijiji kimevamia na watu hao.
Alisema wanakijiji walijitokeza kwenda eneo la tukio na kuwashambulia watafiti hao hadi kufa.
Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana alisema baada ya kutembelea eneo la tukio, ameamua kuwasimamisha kazi kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino na ofisa utumishi wa wilaya hiyo kwa madai ya kutosambaza barua za kuwatambulisha watafiti hao katika maeneo waliyokwenda kufanya kazi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Kawea alisema taarifa alizozipata kutoka kwa diwani wa kata ya Iringa-Mvumi, watafiti hao walipofika katika eneo la Makamwa walikutana na watu na kuwauliza kilipo kijiji cha Iringa-Mvumi.
Kawea alisema watafiti hao walipofika eneo walilotaka kufanya utafiti walipigiwa yowe kwamba ni wanyonya damu.
Alisema baada ya kelele zile wanakijiji waliokuwa katika mkutano walisikia na kutoka na mapanga na silaha za jadi kisha kuwavamia watafiti hao na kuwashambulia kwa silaha hizo.
“Hata walipoonyesha vielelezo wao si wezi bali ni watafiti waliopewa kibali na halmashauri ya Chamwino na vielelezo vingine, wanakijiji walikataa na kuendelea kuwapiga,” alisema.
Alisema watendaji wa kijiji hicho na diwani wa kata hiyo, Robert Chikole waliwasihi wanakijiji kuwaacha watafiti hao lakini walizidiwa nguvu na wananchi.
Aliongeza: “Hata polisi walifika muda mfupi, walikuta wameumizwa vibaya wakarusha risasi juu lakini walizidiwa nguvu na kukaa pembeni. Kwa kweli wamekufa katika tukio la kinyama,” alisema.
Alisema watafiti hao walikwenda katika ofisi za Wilaya ya Chamwino na kupata kibali kabla ya kwenda kijijini hapo kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo.
Alisema diwani, mtendaji na mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Habari kutoka kijijini hapo zinasema wanakijiji wamekimbia makazi yao kutokana na msako wa polisi kwenye eneo hilo.
Majonzi yatawala Arusha
Mauaji ya hayo yameibua simanzi katika taasisi ya Selian na familia zao, ikiwamo ya mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk January Mfuru ambaye mtoto wake pia ameuawa.
Mtoto huyo, Faraji Mafuru amehitimu Chuo cha Mipango Dodoma hivi karibuni na alikuwa katika mazoezi kwa vitendo.
Mratibu wa utafiti katika kituo hicho, Dk Charles Lyamchai alisema tukio hilo limetokea wakati timu ya watafiti wa kituo hicho ikiwa mkoani Dodoma kutekeleza mradi wa kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya kuziingiza kwenye kanzidata ya Taifa.
“Hawa walikuwa kwenye mradi maalumu ambao umeanza mwaka 2014 na wapo wengine watafiti ambao wamesambaa kwenda mkoani Dodoma kwa kazi hii,” alisema.
Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni dereva Nicas Magazine na Mtafiti wa maabara ya udongo, Teddy Lumanga.
“Wapo watumishi 10 huko kutoka hapa kituoni, waliokwenda kutekeleza mradi wa kutambua kiwango cha rutuba kwenye udongo nchini ambao tumeshaukamilisha kwenye wilaya zote za mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Katavi na wilaya ya Kondoa, hili ni jambo la kushtua sana,” alisema.
Alisema watafiti hao walikuwa katika wiki ya pili na hawakuwa wamepata matatizo yeyote tangu wafike Dodoma, baada ya tukio hilo kiongozi wa msafara aliwasiliana na kituo.
Dk Lyamchai alisema kabla ya kwenda huwa wanatoa taarifa kwa kuandika barua kwenye wilaya husika, pia maeneo ya vijijini huwa wanaambatana na mabwana shamba.
“Watafiti wetu hawana mahusiano yoyote na masuala ya damu, walikuwa kwenye kazi zao na walitoa taarifa hadi ofisi ya kata ila hatujui ni kwa nini tukio hili limejitokeza,” alisema.
Mtafiti mwandamizi wa kituo hicho, Dk Lameck Makoye alisema hawajawahi kukutana na changamoto kubwa kama hiyo hasa maeneo ambayo huwa na historia ya wenyeji wasiopenda wageni.
Alisema Dk Mafuru na watafiti wengine waliondoka jana kwendas Dodoma kuungana na watafiti wengine kutoka Kituo cha Hombolo na Makutupola kwenda eneo la tukio.
Selian ni miongoni mwa vituo maarufu katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa kufanya tafiti za mazao katika maeneo yenye ukame nchini.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment