Kafulila alisema serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Mfuko wa Misaada wa Milenia (MCC) imekataa kuidhinisha msaada wa zaidi ya Dola 470 milioni kwa Tanzania kutokana na ufisadi huo.
Harakaharaka akaibuka Saada Mkuya Salum, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi chini ya serikali ya Dk. Jakaya Kikwete, akakana na kumsema Kafulila kuwa anapotosha bunge.
Ikumbukwe wakati huo, tayari Kafulila alishagombana na wakubwa wa serikali hasahasa Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Jaji Fredrick Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, ambaye alimuita mbunge huyo “tumbili.”
Prof. Muhongo na Jaji Werema walikuwa midomoni mwa wabunge wa upinzani kwa kutuhumiwa kuridhia ufisadi wa fedha za Escrow, baada ya kuruhusu zitolewe kwenye akaunti iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusubiri kumalizika kwa mvutano wa Shirika la Umeme (TANESCO) na Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Waziri Saada akilalamika na kumtaka Kafulila afute kauli yake, alisema bungeni, “Si kweli mheshimiwa Spika. Fedha za MCC zitapatikana tukishakamilisha mambo madogo tu yaliyobaki. Hakuna tatizo na fedha hizi, mbunge asipotoshe bunge.”
Kafulila alikataa shinikizo la kufuta kauli, na akashikilia alichokisema.
Ukapita mwezi, miezi na baadaye ikatoka ripoti ya Bodi ya MCC, iliyopitishiwa ofisi ya ubalozi wa Marekani nchini, ikisema msaada umesitishwa mpaka wakati mwingine baada ya masharti kadhaa kutekelezwa, likiwemo la serikali kueleza kwa uwazi fedha zilivyotoka.
Matumaini ya serikali yakaanza kufutika ilipoelezwa na MCC kuwa Bodi imekataa kwa mara nyingine kuidhinisha kutolewa kwa msaada kwa Tanzania. Dhahiri sasa matumaini hayapo tena, maana Bodi ya MCC imeshafunga ofisi zake nchini.
Uamuzi huu mpya umekuja wiki moja baada ya Mahakama ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara iliyoko London, Uingereza kuipa ushindi Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) katika kesi iliyofungua dhidi ya Tanesco, ikidai uhalali wa kumiliki mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL iliyoko Tegeta.
Benki ya Standard Chartered (SCBHK) imeshinda kesi na kuamuliwa ilipwe mamilioni ya dola na kuhalalika kuwa mmiliki wa mitambo hiyo kwani haijalipwa deni lililotokana na kukopesha IPTL fedha zilizotumika kuinunulia.
Mapigo mawili kwa mpigo dhidi ya serikali – kwanza kunyimwa kabisa msaada wa mamilioni ya dola, na pili kulipishwa mamilioni mengine kama adhabu dhidi ya Tanesco iliyoshindwa kesi mahakamani.
Yote haya mawili na athari zake kubwa kwa maendeleo ya nchi, yametokana na ukaidi, uzembe, ubazazi na ujinga wa serikali wenyewe. Iliambiwa haikusikia, iliposikia haikuzingatia, haikuchukua hatua zilizofaa, ikaridhia baadhi ya wakubwa kunufaika kifisadi.
Desturi haitabadilika: Kweli hubakia kweli (haifutiki) na uongo hujitenga. Havitengamani. Niseme haki hubaki haki, kamwe haishikani na batili. Shida ni pale wa serikali ya CCM wasipojifunza.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment