Juzi, Kamati ya Kanuni za Bunge ilihariri hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ikiondoa maneno yanayomtaja Rais John Magufuli na badala yake kuweka neno Serikali kwenye sakata la uuzwaji nyumba za Serikali.
Kamati hiyo pia iliondoa suala la mkataba wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, rushwa, mauaji ya wanasiasa, mwenendo wa Rais na Bunge kulinda wahalifu, jambo lililomfanya msemaji wa kambi hiyo, Godbless Lema kukataa kusoma hotuba yake.
Lakini jana katika hotuba ya kambi ya upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, mbunge wa Vunjo, James Mbatia alilirejesha sakata hilo akieleza kuwa ni muda sahihi kwa Rais John Magufuli kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati akiwa waziri ili kurejesha imani katika jamii.
Mbali na sakata hilo, pia Mbatia alizungumzia sakata la kivuko cha Mv Dar es Salaam ambacho kinatakiwa kifanye safari kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, akikielezea kuwa “ni jipu ambalo limeiva kwa viwango vyote na sasa linatakiwa litumbuliwe mara moja”.
Suala la Mv Dar es Salaam liliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Zitto alisema kuwa hoja ya kivuko hicho lazima ichukuliwe hatua ili iaminike kuwa kuna nia ya dhati ya kupambana na ufisadi nchini.
“Naona suala hili linakwepwakwepwa, hivyo litolewe maamuzi,” alisema Zitto.
Pia mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema suala la Mv Dar es Salaam kuwa iko chini ya kiwango, liliwahi kusemwa na mbunge wa upinzani lakini Serikali ikakataa.
Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) amesema ukweli katika ripoti yake. “Hili suala inabidi liangaliwe kwa kuwa kuna watu wanahitaji kutumbuliwa hivyo hao watu waangaliwe,” alisema Selasini.
Akisoma hotuba ya maoni mbadala ya kambi ya upinzani, Mbatia alisema wakala wa majengo nchini ndiye muhusika mkuu katika kuhakikisha nyumba za Serikali zinakuwa katika hali nzuri kwa watumishi wa Serikali kuishi.
“Katika muktadha huo, kambi ya upinzania inalikumbusha Bunge kwamba kati ya mwaka 2002 mpaka 2004 Serikali iliuza nyumba 7,921 na mpaka mwaka 2008 ilikuwa imejenga nyumba 650 tu,” alisema Mbatia.
Alisema katika biashara hiyo ya kuuza nyumba zilizokuwa mali ya Tamisemi, Serikali ilipata Sh252 milioni lakini sasa inahitaji kusaka zaidi ya mara mbili ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia.
Mbatia alisema Serikali ingetumia Sh677.6 milioni kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe Tamisemi.
“Kwa vile hata wale waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kati yao wapo walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo, kambi ya upinzani inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.”
Mbatia alisema kumbukumbu rasmi za Bunge zinaonyesha Serikali ilitoa taarifa kuwa kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya nyumba hizo na ilitarajiwa kumaliza kazi Februari 2007, lakini hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa na Serikali na kuitaka Serikali ya Awamu ya Tano izirejeshe.
Akinukuu kumbukumbu rasmi za Bunge za Aprili 25, 2008 wakati wa kikao cha 18 cha Mkutano wa 11, Mbatia alisema baada ya mjadala mkubwa wa hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, Bunge kwa kauli moja lilipitisha azimio kuwa nyumba hizo zirejeshwe serikalini.
“Bunge linaazimia kwamba Serikali ifanye yafuatayo: Itekeleze mara moja bila kusita, agizo la Rais kurejesha nyumba zilizouzwa kinyume cha utaratibu na kwa watu ambao hawakuwa watumishi wa Serikali wakati huo na vilevile nyumba ambazo hazikupaswa kuuzwa kama zile zilizopo kwenye maeneo ya utawala wa Serikali,” alisema akinukuu azimio hilo.
Mbatia aliitaka Serikali itafsiri kaulimbiu ya “hapa kazi tu” kwa kuelekeza azimio hilo, akisema Kikwete alikosa uthubutu wa kusimamia msimamo wake.
“Tunajua uuzwaji huo ulisimamiwa na wizara aliyokuwa akiiongoza yeye (Rais Magufuli) na kuna uwezekano mkubwa kwamba alisimamia maamuzi ambayo hakuwa na uwezo wa kuyakiuka,” alisema Mbatia.
“Sasa ni muda sahihi Rais Magufuli kurekebisha kasoro alizozisimamia katika mchakato huo ili kurejesha imani katika jamii.”
Kivuko cha Bagamoyo
Kuhusu kivuko cha Bagamoyo, Mbatia alisema kilinunuliwa na Temesa chini ya uongozi wa Waziri wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Nne ambaye ndiye Rais wa sasa.
Mbatia alisema kwa mujibu wa ripoti ya CAG katika hesabu za Serikali Kuu za mwaka ulioishia Juni 30, 2015 iliyotolewa Machi 2016, alibaini ununuzi wa boti ‘feki’ na mbovu uliofanywa na Temesa na kugharimu dola 4,980,000 za Marekani (sawa na Sh7.9 bilioni).
Alisema CAG alibaini masuala makuu mawili ambayo ni kasi ya kivuko hicho ni tofauti na kasi iliyotakiwa kuwapo na pia cheti cha kukikubali kivuko hicho kilikuwa kinyume na Kanuni ya 247 ya Sheria ya Manunuzi ya Umma.
“Tabibu wa kutumbua jipu hili yuko wapi? Au msemo usemao kuwa ‘mganga hajigangi’ unatumika hapa?” alihoji.
Juzi jioni hali kama hiyo ya kuzungumza masuala yaliyozuiwa na Kamati ya Kanuni za Bunge, ilijitokeza wakati wabunge wakijadili Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Akichangia mjadala huo, Lema alianza tena kuzungumzia suala la Lugumi, akisema kabla ya kuandika hotuba hiyo alikaa pamoja na Waziri Charles Kitwanga wakila ugali nyumbani kwake na kumtaka amwambie ni mambo gani ayajumuishe kwenye hotuba yake ambayo yangeisaidia nchi.
“Haya mambo ambayo mimi nimeyaandika, nimeyajadili nyumbani kwake tukiwa tunakula ugali. Na nakwambia mimi ni mara ya pili kuingia bungeni. Ninazijua siasa za Bunge.
"Ninakuomba mheshimiwa uniambie mimi kama kambi ya upinzani ninaweza kuzungumza mambo gani ambayo Serikali haiwezi kuja nayo direct. Usiponiambia mimi nitakunyookea na nitataka majibu.
“Waheshimiwa wabunge, nimeuliza swali ambalo nimeambiwa na kamati niliondoe, kwamba hivi kamati ya Bunge inapotembelea kote huko kutafuta sakata hili la Lugumi, CAG anashindwa kutwambiwa kama mkataba ule ulikuwa thamani yake ya fedha na vifaa ni OK au ni no, anashindwa kujua?” alihoji Lema huku akishangiliwa.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment