Chadema |
Aidha, maandamano hayo ya nchi nzima imeelezwa kuwa ndio kifo cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwani kila chama kimekuwa kikihangaika kivyake.
“Wanaotaka kuandamana wanajidanganya na kuwalaghai wenzao kwani kufanya operesheni ni suala la dola na si la mtu au kikundi cha watu, hivyo maandamano hayo hayawezekani kabisa,” alisema Profesa Bana katika mahojiano maalumu na Idara ya Habari (MAELEZO).
Mhadhiri huyo Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliongeza kuwa wanaojiita Ukuta ni kwamba Rais John Magufuli amewanyima ajenda, kwani utendaji wake umezidi fahamu zao na kuwafanya waanze kutapatapa wasijue nini cha kufanya.
Alisema kama viongozi wa Ukuta ni waungwana, inabidi watamke wazi kuwa wametafakari na kuona kuwa maandamano hayana maana hivyo wameamua kuyasitisha nchi nzima.
Kuhusu utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, Profesa Bana alisema ni serikali yenye maamuzi ya uhakika na inayowajali watu wote bila kujali itikadi zao za vyama, dini wala makabila hivyo inabidi Watanzania waipende na kuiheshimu.
“Rais Magufuli utendaji wake ni wa kuigwa na viongozi wengi duniani kwani anafanya maamuzi ya uhakika ikiwemo kukuza uchumi kwa kukusanya kodi na kuziba mianya ya ubadhirifu wa mali ya umma,” alisema Profesa Bana.
“Pamoja na kuwa Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa kipindi kifupi, viashiria vyote vinaonesha kuwa ni kiongozi imara na shupavu kutokana na mambo makubwa ambayo ameyafanya kwa kipindi hiki kifupi. Katika kipindi hiki kumekuwepo na nidhamu katika utumishi wa umma, kodi inakusanywa kwa kiwango kikubwa na elimu ya msingi inatolewa bure kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala inavyosema,” alisema Profesa Bana.
Aidha, Profesa Bana alisema kuwa wanaomlaumu Rais Magufuli ni wale ambao hawajitambui na labda wanaona mianya ya ubadhirifu anayoendelea kuiziba, wao wanakosa mapato, vinginevyo Rais anafanya vizuri katika kuliongoza Taifa.
“Rais Magufuli yuko sahihi kwa jinsi anavyosimamia vipaumbele vya serikali ikiwemo elimu bure, kukusanya kodi na kuzuia mianya ya rushwa pia dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda,” alifafanua Profesa Bana.
Aliitofautisha Serikali ya Awamu ya Tano na awamu nyingine zilizopita kwa kutokuwa na kigugumizi katika kufanya maamuzi ikiwemo ya kuhamia Dodoma, kuondoa wabadhirifu katika utumishi wa umma na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na fedha hizo kutumika kwa miradi ya maendeleo kama miundombinu, afya na elimu.
Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR Mageuzi, Leticia Mosore amesema vyama vilivyoko katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimepoteza mwelekeo na vinashindwa kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mosore alisema ujio wa maandamano ya nchi nzima yaliyopewa jina la Ukuta, ndio kifo cha Ukawa kwani kila chama kimekuwa kikihangaika kivyake.
Kuhusu Ukawa kupoteza mwelekeo, alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli inayafanyia kazi kivitendo yale yote ambayo yalikuwa ni kero na matatizo yaliyokuwa yakipigiwa kelele na upinzani, na hivyo ingewapasa sasa kufurahia na kumpongeza kwa dhati kwa hatua hizo.
Alisema Ukawa hivi sasa imekuwa ikitoa matamko ya ajabu, imekuwa kama umoja wa kufanya vituko bungeni kila siku wanatoka na kususa, kufunga midomo, mara wavae nguo nyeusi, na hata kuwatimua wale wanaotofautiana nao.
Katika hatua nyingine, Mosore alisisitiza kwamba hatambui kusimamishwa uanachama na uongozi katika chama hicho na ataendelea kufanya majukumu yake kama kawaida kwa kuwa barua aliyopewa haijatoa sababu za hatua hiyo. Alisema hakupewa haki ya kujitetea kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho ya mwaka 1992.
“Ninachoweza kusema kwa ufupi, sitambui kusimamishwa uanachama kwa sababu sijaelezwa sababu za kusimamishwa kwangu wala barua haielezi vifungu vya kikatiba au kanuni zilizotumika kufikia maamuzi,” alisema Mosore.
Uongozi wa wafanyabiashara ndogo maarufu kama ‘wamachinga’ wa soko la Mwenge jijini Dar es Salaam, umesema hauungi mkono maandamano ya Ukuta kwa kuwa maandamano hayo si halali kisheria. Uongozi huo, umesema maandamano hayo hayana uhalali wa kisheria kwa kuwa tayari Jeshi la Polisi nchini limeyazuia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa soko hilo, Omari Hamisi alisema hawapo tayari kuumizwa na askari Polisi kwa sababu ya maandamano hayo ya Ukuta.
Alisema wafanyabiashara hao wanamuunga mkono Rais John Magufuli kwa kutojihusisha na maandamano hayo na badala yake wataendelea na kazi yao ya kufanya biashara ikiwa ni njia ya kutekeleza kaulimbiu ya rais huyo ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kiongozi huyo, alibainisha kuwa Dk Magufuli tangu aingie madarakani, amekuwa akiwatetea wanyonge hasa wafanyabiashara ndogo hivyo kujihusisha na maandamano hayo ni sawa na kumsaliti. Alisema rais huyo alionesha wazi nia yake ya kutetea wanyonge alivyozungumza hivi karibuni na wananchi wa Mwanza na baadaye Dar es Salaam ambako alielezea mikakati na mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwasaidia na kuwakomboa wanyonge.
“Dk Magufuli ameonesha nia ya dhati kutetea wanyonge sasa leo hii tukiandamana na kuunga mkono maandamano yaliyozuiwa na Polisi ni sawa na kumsaliti,” alisema.
“Ukuta ina maana gani na faida gani kwetu? Nchi yetu ni moja, taifa letu ni moja, sisi ni wamoja hivyo hatukubali kufanya maandamano yasiyo na tija kwetu na taifa pia,” alisisitiza na kueleza kuwa wafanyabiashara hao wameshtuka na kuchoshwa na kitendo cha wanasiasa kuwatumia vijana wachache kwa faida yao binafsi.
Maandamano ya Ukuta yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yakilenga kupinga kile wanachokiita udikteta wa Serikali ya Rais Magufuli yanatarajiwa kufanyika kesho nchi nzima. Polisi na vyombo vingine nchini vimetangaza kuwa maandamano hayo si halali.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment