Kuna mtangazaji wa redio moja ya Arusha amenipigia simu mchana huu kutaka maoni yangu juu ya CUF kumfuta uanachama Profesa Lipumba.
Nikamwambia, kuwa kwa mtazamo wangu, CUF sio tu imefanya kosa, bali imefanya kosa kubwa la kisiasa.
Siasa ni kama mchezo wa mpira, timu moja inaposhinda ni kwa sababu nyingine kuna kosa imefanya. Na hiyo nyingine ikifanya makosa makubwa ya kiufundi, huwa ni tatizo zaidi.
Inasikitisha, kwamba CUF, chama kikubwa na muhimu kwa kukua kwa demokrasia yetu kinafanya maamuzi ambayo yana gharama kubwa ya kisiasa kwa chama hicho.
CUF bado ilikuwa na nafasi ya kutanguliza busara na hekima na kuyapa nafasi mazungumzo kwa kumshirikisha Profesa. Na kama mazungumzo ya usuluhishi, na hapa ni baina ya Maalim Seif na Profesa Lipumba, yangeshindwa, bado, CUF ingeonyesha ukomavu kwa kumpa Profesa nafasi kwenye mkutano mkuu, ajieleze na mkutano mkuu uamue hatma yake.
Na kuna tatizo gani kwa CUF kuwa na Profesa kama mwanachama? Kikundi kidogo cha watu kwenye Chama kinapojenga mazoea ya kuwafukuza wanachama wake na hususan viongozi kwa kutofautiana mitazamo, basi, ni tatizo kubwa.
CUF wamekutana Zanzibar na kumfukuza Profesa. Kwenye karatasi inaonekana kama ni jambo jepesi. Lakini, kwa Profesa huyu huyu , Lipumba, kutangaza hadharani kumfukuza uanachama, kimsingi, CUF wakubali kuwa wachache miongoni mwao wamekiandalia chama chao mazingira ya kuingia kwenye mgogoro mkubwa na hata mgawanyiko.
Demokrasia ya vyama vingi tunayojitahidi kuijenga inaihitaji CUF kama chama imara, na cha pili kwa ukubwa baada ya CCM, Bara na Visiwani.
Bila shaka, CUF haijaishiwa watu wenye busara na hekima, wenye ujasiri wa kuwaambia wenye kukiendesha chama hicho kwa kasi ya kutisha wakiwa kwenye mteremko mkali, kuwa, " Mnakosea".
Maggid.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment