Wasira ajibu:
Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Stephen Wasira amemshukia Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwa mambo manne.
Moja ya mambo ambayo Wasira amesema ni kwamba mbunge huyo wa Chadema hana heshima kwa viongozi wakuu wa nchi.
Wasira alisema hayo baada ya Lissu kudai kuwa alinusurika kupigwa na kada huyo wa CCM wakati wa vikao vya Bunge mjini Dodoma, habari ambayo ilichapishwa jana na Mwananchi.
Akijibu tuhuma hizo, Wasira (pichani) alisema Lissu anaongea kama vile hayuko sawasawa kwa sababu yote aliyoyasema ni uongo, hajui yalitokea wapi na hajui sababu zake.
Wasira alisema hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kumtukana Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, lakini alimshangaa Lissu alipothubutu kufanya hivyo wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema Lissu pia alimtuhumu mambo ya uongo Mwalimu Nyerere kwa kudai alighushi saini ya mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abeid Amani Karume kwenye hati ya Muungano. “Hata wapinzani wenzake walimshangaa,” alisema Wasira.
“Huyu mtu amethubutu kuwatukana maraisi waliopita, kamtukana (Benjamin) Mkapa, kamtukana (Jakaya) Kikwete ambaye alimkaribisha Ikulu na kunywa juisi huku amejikunyata, sasa anamtukana Rais (John) Magufuli. Mimi si msemaji wa Magufuli, lakini huyu Lissu amekuwa anamtukana,” alisema Wasira huku akisisitiza kuwa Lissu hana heshima na maadili.
Wasira alisema kutokana na vitendo hivyo inaonekana Lissu ana matatizo kwa kuwa mtu aliye kamili hawezi kufanya vituko vya aina hiyo.
Pia, alimshangaa Lissu kuwa mstari wa mbele kumsafisha kwa maelezo mazuri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wakati alikuwa wa kwanza kumtuhumu kwa kumuita fisadi kiongozi huyo alipokuwa CCM, akisema huo ni uhalisia wa mtu ambaye mara zote amekuwa hasemi kweli.
“Nashangaa leo ndiye amekuwa mstari wa mbele kumsafisha kwa brashi ya chuma baada ya Lowassa kujiunga nao,” alisema huku akibainisha kwamba hizo ndiyo dalili za mtu asiyesema kweli.
Alisema Lissu kumsafisha Lowassa inaonyesha kabisa kuwa kuna tatizo la ukamilifu kwa mwanasheria huyo mkuu wa Chadema.
“Suala la mwisho Lissu hana maadili…kama atabisha nitatoa ushahidi…” alidai Wasira ambaye amekuwa waziri katika awamu nne za serikali.
Ingawa jana, Lissu hakupatikana, lakini alipozunguma na Mwananchi wiki iliyopita alisema huwa haogopi kusema ukweli.
Source: Mwananchi
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment