Hata hivyo, bure hiyo ni gharama. Baadhi ya abiria waliotumia usafiri wameshapoteza mali zao kwa vibaka, wameumia kutokana na kubanana huku kukiwa na kundi kubwa la wazururaji ambao husafiri na mabasi hayo bila kushuka popote.
Mbali na bughudha kwa abiria, tayari mabasi hayo mapya yameshaanza kuharibiwa baadhi ya vifaa, kutokana na kukosekana ustaarabu kwa watumiaji. Huo ndiyo usafiri wa mabasi yaendayo haraka.
Awali ilikuwa mabasi hayo yatoe huduma bure kwa siku mbili kabla Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuongeza siku nyingine tatu, ili kuwapa abiria nafasi ya kujifunza zaidi huduma hiyo.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi ya abiria walilalamikia kuibuka kwa wimbi la vibaka wa simu na fedha, ambao wamekuwa waking’ang’ania milangoni bila kushuka kwenye vituo.
Mmoja wa abiria aliyeibiwa simu wakati akienda Kariakoo, Richard Frank mkazi wa Mbezi, alisema wizi huo hutokea nyakati za kupanda na kushuka.
“Baada ya kushuka Kariakoo nikagundua simu sina, tatizo linaanzia mlangoni ambako kuna msongamano mkubwa wa watu… ungewekwa utaratibu wa namba ili watu waingie kwa ustaarabu badala ya kujazana,” alisema.
Katika kituo cha Kimara Mwisho, kijana ambaye hakufahamika jina lake alinusurika kuuawa baada ya kukamatwa akitaka kuiba simu kwa abiria waliokuwa wakisukumana kuingia kwenye basi.
“Ilikuwa saa nne asubuhi zilipoibuka kelele za mwizi kituoni, ghafla kijana mmoja alianza kupigwa hata hivyo aliokolewa,”alisema Hamis Juma, mkazi wa Kimara.
Abiria mwingine aliyenusurika kuibiwa baada ya kupiga kelele alipohisi jirani yake anapapasa mkoba wake. Halima Shaban mkazi wa Ubungo alisema wizi huo usipokomeshwa, vibaka wengi zaidi watahamia kwenye mabasi hayo.
Askari wa kituo cha Ubungo, Piles Neuka aliwataka abiria kuwa makini wanaposafiri na kwamba vibaka hao watadhibitiwa zaidi huduma itakapoanza rasmi.
“Kwa sasa abiria wawe makini wanapokuwa kwenye msongamano wa kuingia na kushuka,” alisema Neuka.
Msongamano
Mwandishi wetu alishuhudia msongamano wa watu wanaoingia kwa kusukumana kwenye mabasi hayo huku karibu kwenye kila kituo kukiwa hakuna idadi maalumu ya abiria wanaopaswa kusafiri kwenye basi moja. Baadhi ya abiria walisema hali hiyo ni hatari ikiwa itaendelea kuwapo kwani inatishia usalama wao na kusababisha uharibifu wa mabasi hayo.
Meneja Mawasiliano wa Udart, William Katambi alisema abiria wengi walizoea kusukumana wakati wa kuingia kwenye daladala ndio maana wameshindwa kuiacha tabia hiyo. Hata hivyo, alisema itaisha baada ya mabasi kuongezeka kwa kuwa mengi hayajaingia barabarani.
“Naamini wataacha kwa sababu bado tunaendelea kuwaelimisha, na msongamano utakoma yakishaongezeka,” alisema.
Hali ndani ya basi
Abiria wengi walikuwa wamesimama kwa kubanana kutokana na idadi ndogo ya viti. “Nahitaji kajinafasi ya kuweka miguu tu,sogeeni jamani!” alisema mmoja wa abiria akiomba waliokuwa mlangoni kujisogeza ili naye aingie.
Uharibifu
Dereva wa basi lenye namba T810 DGV alikuwa akilazimika kuwatangazia abiria kuwa mlango mmoja umeharibika hivyo watalazimika kupanda na kushuka kwenye mmoja uliobaki.
“Samahani ndugu abiria, mlango mmoja mbovu hivyo pandeni na kushuka kwenye mwingine uliopo,”alisema dereva.
Pamoja na dereva huyo kuwataka abiria wawe makini na kusubiriana kwenye vituo wengine wanaposhuka ili kuepuka uharibibu huo, waliendelea kusukumana hali ambayo ni hatari.
“Wabongo bwana tumeshazoea kusukumana basi imekuwa tabu, hatuwezi kuvumiliana hata kidogo,”alisema mmoja wa abiria aliyekuwa akishindwa kushuka hivyo kupitiliza kituo.
Katambi aliwaondoa hofu abiria kwa madai kuwa idadi ya magari iliyopo itaondoa msongamano huo.
Usalama wa wanafunzi/watoto
Ule usemi kwamba mtoto wa mwenzako ni wako uliwashinda abiria wengi baada ya kushindwa kuwasaidia watoto wanaopanda mabasi hayo.
Baadhi ya watoto wamekuwa wakijitahidi kupenya huku wakisukumana na wakubwa wanapoingia na kushuka kwenye mabasi hayo.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Msewe, Emilia Pabro aliomba kuwe na utaratibu utakaowasaidia kusafiri bila kuumizwa kwenye mabasi hayo.
Walemavu/wazee/wajawazito
Baadhi ya walemavu walisema mabasi hayo hayatakuwa na msaada kwao kama ilivyo kwa daladala za kawaida.
Mlemavu wa macho, aliyeshindwa kupanda basi hilo kwenye kituo cha Kimara Mwisho, Angella Benson aliiomba Serikali kuweka utaratibu kwa makundi maalumu kupanda bila kusukumwa.
Baadhi ya wagonjwa walishindwa kusafiri na kulazimika kutumia daladala za kawaida baada ya kukosa msaada kutokana na idadi ya watu hasa vituo vya Ubungo na Kimara Mwisho kuwa na msongamano mkubwa wa abiria.
Hofu ya kuambukizana magonjwa
Baadhi ya abiria walisema kuna hofu ya kuambukizana magonjwa kutokana na msongamano wa abiria kwenye mabasi hayo.
Elimu kwenye vituo
Baadhi ya maofisa waliokuwa wakitoa elimu juu ya matumizi ya mabasi hayo, walisema kuna changamoto ya wakazi hao kuelewa haraka mfumo wa malipo.
Kwa mujibu wa maelekezo ya maofisa hao, kila abiria atatakiwa kufuata hatua mbalimbali kabla ya kupanda usafiri huo na kushuka.
Hatua hizo ni kulipa na kupewa kadi ambayo ndiyo itakayotumika kuingia na kutoka katika kituo.
Abiria wote wanapaswa kutumia mlango wa mbele au nyuma wakati wa kuingia kwa kugusisha kadi ambayo ndiyo inayofungua mlango.
Baada ya kuingia, basi linapofika kituoni, milango yake hufunguka sambamba na ilipo ile ya kituoni hivyo kutokuwa rahisi kwa mtu yeyote kupenya.
Katika utaratibu huo, ni vigumu kwa abiria kuingia na kutoka bila kulipa kutokana na mfumo huo.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment