Nov 8, 2016

Zitto Kabwe Afunguka Haya Kuhusu Marehemu Samweli Sitta


Alfajiri ya tarehe 7 Novemba 2016, tunaamka na kukutana na habari za kusikitisha kuwa Mzee Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangulia mbele ya haki. Babu alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo akisumbuliwa na saratani ya tezi dume.


Majonzi ni makubwa kwa Taifa kutokana na sababu kubwa kwamba Samwel John Sitta alitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa.


Sisi wengine pia kwa kiasi fulani kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofahamiana naye binafsi na namna nilivyomshuhudia katika kazi zake.


Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa babu yangu. Tukiwa bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.


Aliniapisha kiapo cha ubunge Desemba 29, 2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyo hiyo jioni.


Baada ya kula kiapo cha utii na cha uaminifu kawaida wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi. Kwa upande wangu Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia, “utakuwa kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future.”


Maneno haya hayajawahi kutoka katika kumbukumbu zangu na kila nikipata misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka na wakati mwingine yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha na kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi wa wanasiasa vijana.


Sitta pia amenilea kwa kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos jijini Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE).


Hali ya hewa ya Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwaumwa sana. Pia nilitaka kusoma Hesabu badala ya Historia. Wakati wa likizo ya Desemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati huo Bwana Ndeki alisoma na Samwel Sitta.


Kipindi hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC). Nikaenda Ofisi za IPC mahali ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe.


Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu dakika chache tu. Akaniruhusu.


Nilipofika Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma akaniambia, “wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yoyote nchini ya chaguo lako”. Akainua simu akampigia Bwana Ndeki. Kisha akaniandikia kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.


Nilipotoka nje ya wizara nikakutana na kijana mwingine anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mzee aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na kumwambia sitaki Mazengo akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua ‘whiteout’ akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “ nyie watoto wa wakubwa bwana”. Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga kusoma Economics, Geography na Mathematics (EGM).


Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.


Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004 ilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za Kijerumani na Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabiashiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.


Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Mzee Sitta akawa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa ofisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo.


Mwaka mmoja baadaye tukakutana na Mzee Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta leo mapema asubuhi (jana). Nimempoteza babu mlezi.


Sitta alikuwa mwana mageuzi (reformer) na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa, tukimwita Spika wa Viwango na Kasi, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanalingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawa sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa katika kuleta mabadiliko hayo.


Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano huo ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo. Si Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi hizo. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.


Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa taarifa za Kamati za Bunge na hususani Kamati za Usimamizi wa Serikali zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.


Wakati wa Bunge la Nane, Taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac ) ilianzishwa Machi, mwaka 2008.


Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa kamati hiyo na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama kamati ya wabunge wazee. Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa Poac nayo ni hadithi nyingine ya namna ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.


Sikuwa nimejaza fomu kuomba Kamati ya Poac. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa na Waziri wa Nishati hotelini nchini Uingereza kwa siri ). Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige.


Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia “Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge. Nimekuteua Kamati ya Poac ambayo ni kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya Mzee William Shelukindo.


Ombi la Mzee ni amri. Nikawa Mwenyektii wa Poac na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Cheyo na Kamati ya Laac ikawa chini ya Dk Wilibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kweli kweli.


Spika Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimsababisha kufanya maamuzi ambayo wakati mwingine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( Epa). Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa wabunge wenye hoja hiyo yaani mimi na Dk Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Waziri Mkuu Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa Serikali. Hoja ya Dk Slaa akaitupa kuwa ‘ ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu bungeni. Wananchi walimkasirikia sana.


Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa Freeman Mbowe Mikocheni, Sitta akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa meseji. Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007, Sitta alijua namna ya kusoma nchi na kuwapa watakacho, wakati mwingine. Mwezi Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na kufuta makosa ya Buzwagi na Epa, Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata yalikuwa historia. Taarifa ya Kamati Teule ilisababisha ‘kuanguka’ kwa Serikali kwa mara ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania, Waziri Mkuu Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza la Mawaziri likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Mizengo Kayanza Pinda.


Spika Samwel Sitta akawa ni Spika pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya uspika wake. Mzee Msekwa yeye alikaa miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye aliona mabadiliko ya mawaziri wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Samwel Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.


Spika Sitta alikuwa mwepesi kuomba msamaha alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza bungeni mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile. Nikaenda kumwona Mzee Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo. Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa ajenda za kawaida tu, Mzee Sitta akamwomba radhi Mzee Cheyo.


Nikikumbuka kisa hiki nacheka sana maana Jaji Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu? Mzee Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema, “John, naomba radhi kwa tukio lililotokea bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe mzee mwenzangu”. Kicheko ukumbi mzima na Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja kitabu, ‘Bunge lenye Meno.’


Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na Viwango Samwel Sitta? Mwanasiasa shupavu, jasiri, mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyeyekevu inapobidi na mwenye uthubutu. Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. Umeondoka duniani lakini bado unaishi kupitia kazi zako kwa nchi yetu.


Mwandishi wa makala haya ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.

Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
Soma Hizi Habari Zetu Kirahisi Kupitia Application ya Simu ya Udaku Special, Bonyeza HAPA
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 [disqus]:

Post a Comment

Follow Us

Popular Posts

Powered by Blogger.

MKRdezign

Blog Archive

Technology

[blogger]
Contact us
Ajirayako.co.tz
E-mail: ajirayako@gmail.com
DISCLAIMER:
This Website |Ajirayako.co.tz| is Not Affiliated In Any Way
With The Companies Whose Vacancies Are Published Here.
AVOID SCAMS
Never Pay to Have Your CV/Application Pushed Forward. Any job vacancy requesting payment for any reason is a scam.

Contact Form

Name

Email *

Message *

Tags

Abdallah Zombe (3) ACT Wazalendo (7) Afande Sele (6) Afya (42) Air Tanzania (11) Ajali (31) Ajira (16) Akson Tulia (4) Alberto Msando (1) Ali Kiba (10) Almaz Ayana (1) Anna Makinda (2) Anthony Lusekelo (1) Arusha (1) Arusha Felix Ntibenda (1) Asha Rose Migiro (2) Askofu Gwajima (6) ATCL (3) Augustine Lyatonga Mrema (4) Aunty Ezekiel (2) Babu Tale (2) Bajeti (1) Bakwata (3) Baletol (1) Bandari (3) Baraka da Prince (2) Bavicha (1) Benjamin Mkapa (1) Benki Kuu Tanzania (1) Bernad Membe (1) Biashara (1) Bodi ya Mikopo (1) Bongo Movies (7) BOT (1) Breaking News (3) Buhari (1) Bungeni (48) Burudani (45) CCM (5) Chadema (20) Charles Kitwanga (3) Chibok (1) Chid Benz (2) Chris Brown (3) Clouds FM (1) CUF (26) Dangote (3) Daniel Ole Njolay (1) Dart (2) David Kafulila (7) Desmond Tutu (2) Diamond Platnumz (18) DJ Fetty (1) Dk. Reginald Mengi (1) Donald Trump (23) Dr Mwaka (1) Dr Mwaka Aacha Vilio Kwa Wagonjwa...Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Septemba 30 (1) DR Shein (2) Dr Slaa (4) Dr. Ramadhan Kitwana Dau (1) Edo Kumwembe (1) Edward Lowassa (30) Elimu (75) EPA (1) Escrow (3) Ester Bulaya (9) Faiza Ally (1) Fast Jet (1) Featured (3) Flaviana Matata (1) Freeman Mbowe (31) Fumanizi (1) Gadner (1) George Masaju Masaju (1) Gerald Hando (1) Godbless Lema (31) Godwin Gondwe (1) Halima Mdee (2) Hamad Rashid (1) Harmonize (3) Hillary Clinton (3) Iddi Amini Dadaa (1) Idriss Sultan (2) Iphone (1) Irene Uwoya (1) Ivo Mapunda (1) Jack Wolper (3) Jaji Francis Mutungi (3) Jakaya Kikwete (13) Jambazi (2) James Mbatia (1) January Makamba (1) JB (1) Jecha Salim (1) Jenerali Ulimwengu (1) Jerry Muro (3) Jeshi la Polisi (32) Jobs (1) John Cheyo (1) John Mnyika (3) John Pombe Magufuli (83) Joseph Kabila (2) Josephine Mshumbushi (1) Joshua Nassari (1) Julieth Kairuki (1) Julius Mtatiro (9) Jussa (1) Kamanda Sirro (1) Kenyan News (14) KFC (1) Kicheko (1) Kigwangalla (1) Kilimo (1) Kinana (3) Kitanzi (1) Koffi Olomide (2) Korea (1) Kuliko Jana (1) Leicester City (1) Livingstone Lusinde (1) Lugumi (1) Lulu Michael (1) Maajabu (3) Maalim Seif (14) Madam Rita (1) Madawa ya Kulevya (7) Magazeti (49) Mahakamani (7) Mai Mai (4) Maisha (2) Majambazi (7) Makahaba (1) Makalio Makubwa (1) Makamba (1) Malaika (1) Malezi (1) Mama Salma (1) Man Fongo (2) Man United (1) Mange Kimambi (2) Manji (7) mape (1) Mapenzi (76) Marcus Rashford (1) Mashine ya MRI (1) Matiko (1) Matokeo (3) Mauaji (31) Mauji (2) Mbeya (2) Mbunge Lusinde (1) Mbwana Samatta (8) Mchungaji Anthony Lusekelo (1) Meya wa Kinondoni (1) Michael Shirima (1) Michez (1) Michezo (201) Miss Tanzania (2) Mizengo Pinda (1) Mongela (1) Mr Blue (3) Mrema (7) Mrisho Gambo (3) Mrisho Mpoto (2) Msigwa (2) Mugabe (1) Museven (1) Music (85) Muungano (1) Mwakyembe (2) Mwanafunzi (3) Mwendokasi (1) Mwigulu Nchemba (2) Nape Nnauye (13) Navy Kenzo (1) Nay wa Mitego (2) Ndanda FC (1) Ndugai (1) Necta (3) Nida (1) Nigeria (2) NSSF (1) Nuh Mziwanda (2) Nyerere (1) Obama (9) Ommy Dimpoz (2) Original Comedy (2) Oscar Pistorius (1) Paul Makonda (34) Paul Pogba (2) Pep Guardiola (1) Peter Msigwa (4) Petitman (1) Polisi (4) Pombe (1) Pride (1) Prof Mkumbo (2) Prof. Benno Ndulu (1) Prof. Ibrahim Lipumba (12) Prof. Lipumba (23) Prof. Tibaijuka (3) Profesa Benno Ndulu. (1) Profesa Muhongo (3) Q-Chief (1) Raila Odinga (2) Rais Magufuli (35) Ray C (1) Reginald Mengi (2) Rihanna (1) Robert Mugabe (4) Ruby (5) Rushwa (3) Sadaka (1) Saed Kubenea (3) Saida Karoli (2) Salama Jabir (1) Salum Mwalimu (2) Samia Suluhu (1) Samsung Galaxy (1) Samwel Sitta (5) Sauti Sol (1) SBL (1) Scorpion (3) Serengeti Boys (1) Shamsa Ford (2) Sheikh Abubakar Zubeiry (2) Shibuda (2) Shilole (1) Siasa (1945) Siasa Huru App (3) Siasa za Kenya (1) Simba (1) Slaa (1) Snura (1) South Africa (1) Sudan (1) Sugu (1) Sukari (4) Sumaye (8) Supu ya Pweza (1) Tanesco (9) Tanzia (22) TB Joshua (4) TBS (1) TCRA (5) TCU (4) Technology (3) Tetemeko (13) TFDA (1) Thereza May (1) Thomas Mashali (1) TRA (4) Tundu Lisu (20) Tyrant (1) Ubakaji (4) Uchambuzi (1) Uchawi (1) Uchumi (90) Udaku (46) Udaku Spesho (21) UDSM (1) Ufisadi (2) Ugaidi (6) Uhuru Kenyatta (2) Ujambazi (4) Ujauzito (1) Ukahaba (1) Ukatili (1) Ukawa (11) Ukuta (11) Ummy Mwalimu (1) Urembo (15) Ushirikina (1) Utafiti (2) Utapeli (3) UVCCM (4) Vioja (1) Wastara (1) Watumishi Hewa (1) Waziri Mahiga (2) Waziri Mkuu Majaliwa (18) Wema Sepetu (6) Wiliam Lukuvi (6) Yanga (7) Yaya Toure (1) Zitto Kabwe (33) Zuckerberg Mark (1)

Categories

Advertisement

Main Ad

Facebook

Responsive Ads Here

Featured

Recent

Udaku Special Test

Copyright © Udaku Special Test | Powered by Blogger