Wiki iliyopita, Millya alitoa tuhuma dhidi ya kampuni hiyo akidai inalindwa na baadhi ya mawaziri, huku akilitaja jina la Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), kuwa ana ushemeji na mmoja wa wabia wa kampuni hiyo, jambo linalowapa kiburi cha kufukuza watumishi bila kuchukuliwa hatua.
Tuhuma hizo zilimuinua Waziri Mhagama akiomba mwongozo wa Spika, kutaka Millya athibitishe anayoyasema au afute kauli yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Akitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Waziri Mhagama, Naibu Spika, Tulia Ackson alisema Millya alitoa madai hayo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Akinukuu maneno ya Millya kama yalivyo kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge) alisema: “Sheria za kazi zinajulikana ni bahati mbaya kwamba mama yetu Mhagama naye anatajwa kwamba, ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusuf Mhagama.”
Baada ya maelezo hayo, Dk Tulia alisema Mhagama aliomba mwongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni ya 64(1), inayoeleza kuwa bila kuathiri Ibara 100 ya Katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, mbunge atatoa taarifa bungeni ambazo zina ukweli.
Dk Tulia alimtaka Millya kufuta kauli yake dhidi ya Waziri Mhagama, au kama anao ushahidi wa kuthibitisha kauli yake autoe kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge.
Millya alisema ni kweli alitaja jina la Waziri Mhagama, na ana ushahidi wa watu wanaomtaja kwenye ujumbe wa simu.
Dk Tulia alimwambia Millya kuwa amemwelewa na kumpa siku nne kuanzia jana, kuthibitisha ushemeji wa waziri na mtu ambaye alimtaja kwenye uwasilishaji wake.
Bonyeza Play Hapa Chini Kuona Walichofanya Bilnass na Rosa Ree:
0 [disqus]:
Post a Comment